6 Septemba 2021 - 08:44
Sudan: Hatutaruhusu ardhi yetu itumiwe na wengine; hatuna mpango wa kuhujumu ardhi ya taifa jingine

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan ameonya kuhusiana na njama dhidi ya taifa hilo na kusema kuwa, nchi hiyo haitaruhusu ardhi yake kutumiwa na wengine na kwamba, Khartoum haina mpango wa kufanya hujuma na mashambulio dhidi ya ardhi ya taifa jingine

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Dr. Mariam al-Sadiq al-Mahdi amesema kuwa, anatoa wito wa kusitishwa uadui dhidi ya Sudan unaofanyika kwa maslafi binafsi ya kundi fulani la watu.

Kadhalika amesema kuwa, kila mara Ethiopia inapokabiliwa na matatizo ya ndani huinyooshea kidole Sudan na kuionyesha kuwa ni msababishaji wa matatizo hayo hali ya kuwa si kweli.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Sudan ameitahadharisha Ethiopia na kuitaka iachane na sera zake za kuendesha uadui dhidi ya Sudan.

Wasiwasi katika mpaka wa Sudan na Ethiopia uliongezeka baada ya kutokea mapigano katika eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka jana (2020). Zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia walikimbilia katika maeneo ya mashariki mwa Sudan kukwepa mapigano hayo.

Ugomvi baina ya Sudan na Ethipia unahusiana na maeneo ya kilimo katika eneo la al Fushqa hasa baada ya wakulima kutoka Ethiopia kuyavamia maeneo hayo ya Sudan.

Hivi karibuni kuliripotiwa kutokea mapigano ya silaha baina ya wanajeshi wa Sudan na Ethiopia huku kila upande ukiushutumu upande mwingine kuwa ndio ulioanzisha mapigano hayo. Hivi karibuni pia nchi hizo mbili zilifanya mazungumzo mjini Khartoum kwa ajili ya kutatua mgogoro huo.

342/